Pages

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

Saturday, August 26, 2017

WAZIRI MKUU ATEMBELEA KIWANDA CHA KUZALISHA SUKARI NCHINI CUBA


Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akipata maelezo ya ukarabati wa kiwanda cha Sukari cha UGB  kutoka kwa Mkurugenzi Mkuu wa Bodi ya Sukari nchini Cuba Bwana Francisco Martin, jana August 24/2017 kiwanda hicho kipo katika Mji wa San Nicola's de Bari nchini Cuba
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akiangalia shehena ya sukari iliyozalishwa katika kiwanda cha UGB Central Azucarero 30 Noviembre wakati alipotembelea kiwanda hicho jana August 24/2017 kilichopo katika mji wa San Nicola's de Bari nchini Cuba.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amekutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Shirika la Viwanda vya Sukari nchini Cuba, Bw. Francisco Lled, ambaye amekubali kushirikiana na Serikali ya Tanzania katika kuongeza uzalishaji wa sukari nchini.

Shirika la Sukari la nchini Cuba linauwezo wa kuzalisha tani milioni nne za sukati kwa mwaka huku mahitaji ya ndani ni tani 700,000, ambapo kiasi kinachobaki huuzwa nje ya nchi. Kwa sasa shirika hilo linazalisha tani milioni mbili tu katika viwanda vyake 56.

Waziri Mkuu alikutana na Bw. Lled jana (Alhamisi, Agosti 24, 2017), wakati alipofanya ziara katika kiwanda cha kuzalisha sukari cha UGB Central Azucarero 30 de Noviembre katika mji wa San Nicola’s de Bari ambacho ni kati ya viwanda 27 vya shirika hilo linalomilikiwa na Serikali ya Cuba kwa asilimia 100.

Katika mazungumzo yao Waziri Mkuu alimshawishi Bw. Lled kuja nchini kwa ajili ya kuwekeza katika ujenzi wa viwanda vya kuzalisha sukari. Alisema kwa sasa Tanzania kuna viwanda vikubwa vitano vya sukari ambavyo uzalishaji wake hautoshelezi mahitaji ya ndani.

Waziri Mkuu alivitaja viwanda hivyo ambavyo ni Mtibwa na Kilombero (Morogoro), Mahonda (Zanzibar), TPC (Kilimanjaro) na Kagera ambavyo vyote vinazalisha jumla ya tani 320,000 za sukari kwa mwaka huku mahitaji yakiwa ni zaidi ya tani 400,000.

Hata hivyo, Waziri Mkuu alisema Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi inatarajia kujenga viwanda vitatu vya kuzalisha sukari, ambavyo vitazalisha sukari itakayotosheleza mahitaji na ndani ya nchi na kiasi kitakachosalia kitauzwa nje.

0 comments: