Rais Jakaya
Mrisho Kikwete ameitaka Jumuiya ya Kimataifa kuhakikisha kuwa malengo
ya milenia yanatekelezwa kwa ukamilifu hata baada ya kuisha muda
uliowekwa wa kuyatimiza, kabla ya kuweka malengo mengine duniani.
Rais
Kikwete ametoa ushauri huo tarehe 28 Mei,2014 mwanzoni mwa mkutano wa
kimataifa unaohusu Afya ya Mama na Mtoto jijini Toronto Canada, ambapo
alikuwa akijibu maswali kuhusu matokeo ya malengo ya milenia kuelekea
mwisho wa muda wa kuyatekeleza mwakani 2015.
“Tukamilishe pale ambapo hatujamaliza na kuimarisha yale yote tuliyoyafanikisha au kuyafikia
” Rais amesema na kuwataka Mataifa kuhakikisha kuwa, malengo manane (8)
ya milenia waliyojiwekea, yanatekelezwa,kwa ukamilifu kwani ni malengo
mazuri na muhimu kwa jamii zetu.
Rais amesema “baada
ya kuyaimarisha na kuyatimiza haya malengo manane tunaweza kupanga na
kutafuta mengine na pia tuhakikishe kuwa haya ya sasa hayasahauliki wala
kutelekezwa ili tusije kurudi nyumba katika jitihada zetu”.
Malengo ya
Milenia Kama yalivyoainishwa na Umoja wa Mataifa ambayo nchi
zinazoendelea zinatakiwa kuwa zimeyafikia ifikapo mwaka kesho wa 2015 ni
pamoja na kuondoa umaskini uliokithiri na njaa, Elimu ya Msingi kwa
wote, Usawa wa kijinsia na fursa sawa kwa wanawake, kupunguza vifo vya
watoto wachanga na upatikanaji wa huduma bora za uzazi.
Mengine ni kupanga na ukimwi, Malaria na magonjwa mengine,kulinda mazingira na kujenga mshikamano wa kimaendeleo duniani.
Mapema
tarehe 28 Mei,2014, Rais alikutana na wafanyabiashara na wawekezaji wa
makampuni mbalimbali ya Canada, ambayo baadhi tayari yana vitega uchumi
nchini Tanzani.
Rais amewaeleza wawekezaji fursa ambazo wanaweza kupata iwapo watawekeza Tanzania ikiwemo katika sekta mbalimbali za kiuchumi.
Tarehe 29
Mei,2014 mkutano huu unatarajiwa kuendelea na kuzungumzia njia
mbalimbali ambazo Mataifa yanatakiwa kufanya kwa pamoja katika jitihada
zao za kuimarisha Afya ya Mama na Mtoto.
Imetolewa na;
Premi Kibanga,
Mwandishi wa Habari wa Rais Msaidizi,
Toronto-Canada.
29 Mei, 2014
29 Mei, 2014
0 comments:
Post a Comment