Pages

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

Sunday, September 28, 2014

Wake wa Marais pamoja na viongozi wtakiwa kuchukua hatua ili kuhakikisha watoto, wasichana na wanawake wanapata afya na elimu‏

Na Anna Nkinda – Maelezo, New York
  Wake wa Marais pamoja na viongozi wametakiwa kuchukua hatua, kutumia sauti zao na nafasi yao ili kuhakikisha watoto,  wasichana  na wanawake wanapata elimu na afya bora na hivyo kujikwamua na hali ngumu ya maisha.

Mwito huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwenye mkutano uliojadili jinsi gani Dunia ichukue hatua kwa ajili ya afya na uchumi wa wanawake na wasichana uliyofanyika katika ukumbi wa mikutano uliopo Jengo la Umoja wa Mataifa (UN) mjini New York.

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema upatikanaji wa elimu bado ni tatizo kwa watoto wa kike hasa katika nchi zinazoendelea lakini kama watapatikana  watu wa kuwasemea na kuhakikisha watoto hao wanasoma watakuwa wamewasaidia kuwa na maisha mazuri hapo baadaye.

Alisema upatikanaji wa huduma za afya na  elimu bora kwa wasichana kutawasaidia  kujikwamua na hali ngumu ya maisha kwakuwa mwanamke ni mlezi wa familia hivyo basi akiwa na elimu bora hata watoto wake wataweza kusoma na  kubadilisha maisha ya jamii zao.

Akizungumzia kuhusu Taasisi ya WAMA alisema aliamua kuianzisha ili aweze kuwasaidia wanawake na watoto wa Tanzania hivyo basi wanatoa ufadhili wa masomo kwa watoto wa kike ambao ni yatima na wanaoishi katika mazingira hatarishi.

“Kwa upande wa afya tunafanya kazi ya kuimarisha afya ya mama na mtoto kwa kutoa vifaa tiba katika vituo vya afya, Zahanati na Hospitali, kutoa elimu na kuhamasisha jamii juu ya  upimaji wa hiari wa ugonjwa wa Ukimwi na saratani za matiti na shingo ya kizazi”.

Pia tunawawezesha wanawake kiuchumi kwa kuwapa elimu ya ujasiriamali na kuwaongezea mitaji katika vikundi vyao vya ujasiriamali jambo ambalo limewafanya waweze kufanya shughuli mbalimbali za uzalishaji mali na kuongeza kipato cha familia”, alisema Mama Kikwete.

Akiwakaribisha wake wa marais waliohudhuria mkutano huo  Mke wa waziri mkuu wa Belize Dean Barrow, Mama Kim Simplis Barrow alisema wake wa marais wananafasi ya kufanya kazi ya kuisaidia jamii yao hasa kina mama na wasichana ambao wameachwa nyuma kimaendeleo ukilinganisha na wanaume.

Mama Barror alisema ili wake hao wa marais waweze kufanya kazi wanahitaji kupata rasilimali fedha na watu na kuwataka wadau waliohudhuria mkutano huo kushirikiana kwa pamoja ili kuhakikisha wanawake wanapata haki zao za msingi zikiwepo za afya na elimu.

Alisema, “Wanawake wengi wanapoteza haki yao ya kupiga kura kama tutamia sauti zetu na kuwaelimisha wataweza kupiga  kura, kupata huduma bora ya afya na hivyo kuweza kuchangia na kushiriki katika shughuli mbalimbali za maendeleo katika nchi zetu”.

Kwa upande wake Rais wa zamani wa Malawi ambaye alihudhuria mkutano huo kama mwanamke mashuhuri Barani  Afrika Joyce Banda aliwataka wake hao wa marais kuwekeza  na kuwasaidia  wanawake na watoto kwani Mwenyezi Mungu amewapa nafasi hiyo makusudi na  wakifanya hivyo matokeo yake yataonekana nanimwanzo wa kupata viongozi wazuri kwa siku zijazo.

Rais Banda alisema karibu Dunia itasherehekea  miaka 20 tangu mkutano wa kimataifa wa wanawake ufanyike  Beijing nchini China ambao uliweka mwelekeo wa hatua za usawa wa kijinsia na mafanikio yamepatikana kwani kwa sasa wanawake wananguvu na wameweza kushika nafasi mbalimbali za uongozi tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma.

“Nyie mnawakilisha watu wengi, fungeni mambo yanayoondoa usawa wa jinsia kwani matatizo ya wanawake Duniani kote yanafanana. Takwimu zinaonyesha wanawake wanachangia uchumi wa Duniani kwa asilimia 70 lakini ndiyo waathirika wakubwa wa umaskini kwakuwa  wengi wao wanauchumi mbovu”.

Wekezeni zaidi kwa wanawake na wasichana hili liwe ni suala la kitaifa ili wapate  elimu ya msingi, sekondari na vyuo kwani wanaume wanapewa elimu zaidi kuliko wanawake. Wasichana wengi hawaendi shule kwa ajili ya umaskini lakini wakipata elimu wataepukana na ndoa za utotoni”, alisema Rais huyo Mstaafu.

Aliendelea kusema hivi sasa mwanamke akipata ujauzito  hajui kama atapona au atapoteza maisha  hiyo si sawa mwanamke lazima ajifunguea salama na mtoto wake aishi. Aliwataka kuchukua  hatua na kutoa  kipaumbele katika kuimarisha afya ya mama mjamzito na watoto.

Mama Banda alitumia nafasi hiyo kumpongeza Mama Kikwete kwa kazi anayoifanya ya kuwasaidia wanawake, wasichana  na watoto wa Tanzania kwa kutatua matatizo yanayowakabili yakiwemo ya afya, elimu na uchumi.

Mkutano huo ulihudhriwa na wake wa marais kutoka mataifa mbalimbali Duniani, wawakilishi wa mashirika yanayofanya kazi chini ya ofisi za UN, watu na Asasi mbalimbali za Serikali na za kiraia zinazofanya kazi za  kuwainua wanawake na kusimamia usawa wa kijinsia uliandaliwa na mke wa waziri mkuu wa Belize Mama Kim Simplis Barrow ambaye ni mwakilishi maalum wa kina mama na watoto na Balozi wa michezo maalum ya Olympics tangu mwaka 2008.
Mwisho.

0 comments: