Pages

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

Friday, September 26, 2014

Ushirikiano wa pamoja unatakiwa ili kuhakikisha wagonjwa wanaougua saratani wanapata matibabu‏

Na Anna Nkinda – Maelezo, New York
 Ushirikiano wa pamoja unatakiwa ili kuhakikisha wagonjwa  wanaougua saratani za mlango wa kizazi, matiti na  tezi dume wanapata matibabu kwa wakati na hivyo kupunguza idadi ya vifo vinavyotokana na ugonjwa huo.

Rai hiyo imetolewa leo na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akiongea kwenye mjadala wa wake wa marais wa Afrika wa kupambana na saratani za mlango wa kizazi, matiti na tezi dume uliofanyika katika kituo cha Ubunifu cha Jamii kilichopo mjini New York. 

Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema sababu zinazoufanya ugonjwa huo kuua watu wengi ni uelewa mdogo wa jamii kuhusu ugonjwa huo, hakuna ukusanyaji sahihi wa takwimu kwani wagonjwa wengi wanafia majumbani na wanaofika Hospitali kupata matibabu ni wachache, upungufu wa vifaa tiba na wataalamu wa afya waliobobea katika magonjwa hayo.

Akizungumzia kuhusu ugonjwa wa saratani ya mlango wa kizazi alisema ni moja ya ugonjwa unaoongoza kuua wanawake wengi hii ni kutokana na mahusiano yaliyopo baina ya ugonjwa huu na Ugonjwa wa Ukimwi. 

“Licha ya kuwa ugonjwa huu unaua wanawake wengi kila mwaka, lakini kutokana na utaalam uliopo unazuilika na kutibika kama mgonjwa atafanyiwa uchunguzi na kupata matibabu mapema kabla ya tatizo halijawa kubwa na hivyo kupungua vifo vya wanawake ambao ni walezi wa familia”, alisema Mama Kikwete.

Mwenyekiti huyo wa WAMA alisema kwa kushirikiana na Chama cha Madaktari Wanawake Tanzania (MEWATA) wameweza kupambana na saratani za wanawake kwa kufanya kampeni ya kuhamasisha wanawake ili wajitokeze kwa wingi kupima na kutoa elimu kwa jamii ili iweze kutambua dalili za ugonjwa huo na hivyo kupunguza vifo vya wanawake. 

Alisema Tanzania inatumia rasilimali nyingi kupambana na ugonjwa huu, kuzuia maambukizi mapya ya Virusi Vya Ukimwi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, kutoa elimu kwa jamii ili iweze kuufahamu ugonjwa wa Ukimwi na kuchukua hatua ikiwa ni pamoja na upimaji wa hiari na kwa wale ambao watakutwa na ugonjwa watatumia dawa za kurefusha maisha. 

Kwa upande wa wadau wa afya na elimu waliohudhuria  mjadala huo walisema kuna haja ya Serikali za Afrika kutilia mkazo na kuchukua hatua zaidi dhidi ya magonjwa ya saratani za wanawake kwani yanaua wanawake wengi ambao ni walezi wa familia na rasilimali ya taifa.

“Wanawake na wasichana wanatakiwa waelimishwe, wafanyiwe uchunguzi na kupewa matibabu ili waweze kuwa na afya bora kwani  saratani za wanawake ni magonjwa yanayowasumbua wanawake wengi Duniani”, walisema. 

Waliendelea kusema wake wa Marais kwa kazi za kijamii wanazozifanya wanaweza kuimarisha  afya za mama, watoto na wasichana katika nchi zao. Waliwaomba wawasaidie ili kuhakikisha wanapata matibabu.

Tafiti zilizofanyika mwaka 2010 zinaonyesha nchini Tanzania kila mwaka wanawake 6200 wanakutwa na ugonjwa wa saratani  ya mlango wa kizazi  hawa ni asilimia 10 ya wagonjwa wote wanaoweza kuhudhuria Hospitali kwa ajili ya kupata huduma na matibabu kati ya hao 4000 wanapoteza maisha. 


0 comments: