Na Anna Nkinda – Maelezo,
New York
22/9/2014 Zaidi ya
wasichana milioni 58 Duniani wameolewa wakiwa na umri wa chini ya miaka 18
kati ya hao milioni 15 wana umri wa kati ya miaka 10 hadi 14 jambo linalowasababisha
kupata maambukizi ya Ugonjwa wa Ukimwi na kufanyiwa ukatili wa kijinsia.
Kwa upande wa Tanzania
takwimu zinaonyesha kuwa wasichana wanajihusisha mapema zaidi katika mapenzi
ukilinganisha na watoto wa kiume kwani asilimia 13 ya wasichana wanaanza
kufanya mapenzi wakiwa na umri wa chini ya miaka 15 wakati kwa upande wa wavulana
ni asilimia saba.
Hayo yamesemwa leo na
Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Mama Salma Kikwete wakati akifungua
mkutano uliojadili elimu ya afya ya uzazi na jinsia kwa vijana ulioandaliwa na Waziri
wa Ushirikiano wa Kiuchumi na Maendeleo wa Ujerumani Gerd Mueller na kufanyika
katika ofisi za ubalozi wa nchi hiyo uliopo mjini New York nchini Marekani.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema kutokana na kitendo
cha wasichana kujihusisha na mapenzi wakiwa na umri mdogo wamekuwa wakikabiliwa
na tatizo la mimba za utotoni na hivyo wengi wao kushindwa kupata elimu.
“Nchini Tanzania kati
ya msichana mmoja hadi wanne wenye umri wa kati ya miaka 15 hadi 19 wana mimba au watoto , takwimu hizi ni kubwa zaidi katika
nchi zingine za kanda ya Afrika ya Mashariki na Kusini”.
Idadi hii inaonyesha wasichana
wataendelea kuwa kundi lililoathirika kwa kukosa haki zao za kupata afya, watakabiliana
na unyanyasaji na maisha yao yataisha mapema. Tukichukua hatua ya kuwasaidia
sasa tutaokoa wasichana wengi na
kuwasaidia kuwa na maisha mazuri hapo baadaye”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti huyo wa WAMA
alisema vijana wa Afrika wanatakiwa kupewa elimu ya maisha, afya ya uzazi na
usawa wa jinsia ambayo itaendana na mila na desturi zao ili waweze kuwa na
uchaguzi mzuri wa maisha yao kwani theluthi ya idadi ya watu wanaoishi nchi
zilizopo Kusini mwa jangwa la Sahara ni vijana wa kati ya miaka 20 na 24.
Mama Kikwete alisema, “Afrika
ya baadaye na ukubwa wa Dunia inategemea na jinsi tutakavyowaandaa vijana
kujenga maisha yao ya baadaye. Hii itawezekana kama tutawasaidia kuchagua njia
nzuri kuhusu afya yao na kuwaokoa kutoka katika tabia hatarishi”.
Kutimiza hili
tunahitaji kuwa na elimu bora ili mambo ya afya ya uzazi na stadi za maisha yapewe
kipaumbele na uangalizi mkubwa unatakiwa kwa watoto wa kike”.
Akiwakaribisha wadau wa
elimu na afya waliohudhuria mkutano huo Waziri wa Ushirikiano wa Kiuchumi na
Maendeleo wa Ujerumani Gerd Mueller alisema kwa zaidi ya miaka 20 Serikali yake
imekuwa ikifanya kazi ya kuhakikisha vifo vya kina mama wajawazito na watoto vinapungua
na upatikanaji wa huduma ya uzazi wa mpango inaimarika.
“Jambo la ziada
linatakiwa kufanyika hasa katika Bara la Afrika lenye matumaini tutaongeza
ushirikiano tukilenga zaidi katika elimu hasa elimu ya ufundi kwa wasichana na
wavulana”.
Tunahitaji kufanya
jambo la ziada kama tunataka kufanikiwa katika afya na elimu kwa vijana hasa
wasichana. Wasichana wengi wenye umri wa chini ya miaka 18 katika nchi
zinazoendelea wanapata mimba zinazowaletea matatizo yanayopelekea vifo vyao”,
alisema Mueller.
Alisema Serikali ya
Ujerumani itatoa fedha zingine Euro milioni 3 kwa ajili ya na kuandaa programu
za pamoja ambazo zitaongeza elimu ya afya ya
ujinsia na huduma za afya ya uzazi kwa vijana katika nchi za ukanda wa
Afrika ya Mashariki na Kusini.
Akichangia mada katika mkutano huo Mkurugenzi
wa Kanda ya Mashariki na Kusini mwa Afrika kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa
la Kupamba na Ukimwi (UNAIDS) Prof.
Sheila Tlou alisema vijana wanahitaji kupata elimu ya afya ya uzazi na jinsia
ili waweze kujikinga na ndoa za utotoni na Ugonjwa wa Ukimwi.
Takwimu zinaonyesha kwa kila saa moja kuna
maambukizi mapya 50 ya HIV kwa vijana hii ina maana kuwa kwa mwaka kuna
maambukizi mapya 430000. Kwa sasa kuna vijana milioni 2.6 wanaoishi na Virusi
Vya Ukimwi (VVU).
Prof. Tlou alisema
mwaka mmoja umepita tangu Mawaziri wa Afya
na Elimu kutoka nchi 21 za Mashariki na Kusini mwa Afrika wakubaliane maazimio ya
kuongoza juhudi za kuandaa mazingira salama na wezeshi kwa makuzi ya vijana
katika nchi zao.
“Ni muhimu kuyafanyia kazi maazimio hayo
ambayo yatawasaidia vijana kupata elimu
kuhusiana na afya ya uzazi na jinsia jambo ambalo litawasaidia kufahamu zaidi ugonjwa Ukimwi”, alisema Prof. Tlou.
Mkutano huo ambao pia
ulihudhuriwa na Mke wa Rais wa Malawi Gertrude Mutharika ni moja ya maandalizi
ya Mkutano wa 69 wa Umoja wa Mataifa
(UN) utaofanyika hivi karibuni mjini humo.
0 comments:
Post a Comment