Na Anna Nkinda – Maelezo, New York
24/9/2014 Ukosefu wa uelewa na
imani potofu miongoni mwa wanajamii ni moja ya chanzo cha unyanyapaa
kwa watoto wenye tatizo la usonji (Autism) .
Hayo yamesemwa jana na Mke wa Rais Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Mama Salma Kikwete wakati akiongea na Prof. Andy Shih ambaye ni Makamu wa Rais mwandamizi wa Mambo ya kisayansi kutoka Taasisi ya Kimataifa ya Autism Speaks yenye makao yake mjini New York.
Mama Kikwete ambaye pia
ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema jamii bado
haina uelewa kuhusu tatizo la usonji kwani kuna baadhi ya watu wanahusisha
tatizo hilo na mambo ya ushirikina lakini kama jamii itakuwa na uelewa tatizo
la unyanyapaa litapungua au kwisha kabisa.
Alisema usonji bado ni
tatizo nchini Tanzania na nchi zingine lakini wazazi wengi wanaona aibu kusema
hadharani wana watoto wenye matatizo hayo
na hivyo kuwa vigumu kwa watoto hao kupata huduma muhimu ikiwemo elimu.
“Tunatakiwa kufanya kazi kwa pamoja
na wataalamu waliobobea katika taaluma hii ili kuhakikisha jamii inakuwa na uelewa kuhusu tatizo hilo
kwa kufanya hivyo watoto hawa watapata huduma za muhimu kama elimu na afya”,
alisema Mama Kikwete.
Kwa upande wake Prof. Shih alisema Taasisi
yake iko tayari kufanya kazi na WAMA ili kuwasaidia watoto wenye tatizo la
usonji ili waweze kupata elimu na huduma ya afya kama watoto wengine.
Prof. Shih alisema tatizo la
unyanyapaa bado ni kubwa kwa watoto lakini kama jamii itapata elimu na
kulifahamu tatizo hilo itaweza kuwasaidia watu wenye matatizo hayo na hivyo kupunguza
tatizo la unyanyapaa.
Usonji ni hali ya
udhaifu katika ukuaji wa ubongo ambayo huleta athari kubwa katika mawasiliano,
mahusiano ya kijamii na utambuzi.Tatizo hili ni la dunia nzima na bado hakuna
maelekezo kamili ya chanzo chake wala tiba.
Wanaoathirika zaidi ni
watoto wa kiume kuliko wa kike kwa uwiano wa nne kwa moja hii ikiwa na maana
kuwa kila watoto watano wenye usonji wanne ni wa kiume na mmoja wa kike.
Mwaka 1997 wizara ya
Elimu na Utamaduni ikishirikiana na wanachama wa National Association for
People with Autism in Tanzania (NAP-T) walianzisha kitengo cha watoto wenye
usonji katika shule ya msingi Msimbazi Mseto ambacho ni kitengo mama cha kutoa
huduma.
Hivi sasa Serikali
inavitengo vitano, viwili vipo Dar es Salaam, viwili Arusha na kimoja Morogoro.
Pia kuna vitengo kadhaa vilivyoendeshwa na watu binafsi.
0 comments:
Post a Comment