Pages

Sikiliza Tone Radio Live Hapa, na Tembelea Website yetu www.toneradiotz.com

Monday, September 4, 2017

NCHI SITA KUSHIRIKI MASHINDANO YA KUOGELEA YA KANDA YA TATU AFRIKA


Jumla ya nchi sita zimethibitisha kushiriki katika mashindano ya kuogelea ya kanda ya tatu ya Afrika (Cana zone 3) yaliyopangwa kufanyika jijini Dar es Salaam kuanzia Oktoba 19 -21.

Mwenyekiti wa kamati ya maandalizi ya Chama Cha kuogelea nchini (TSA), Leena Kapadia amezitaja nchi hizo kuwa ni Afrika Kusini, Zambia, Kenya, Uganda, Djibouti na wenyeji Tanzania.

Kapadia amesema kuwa walitarajia kuona nchi nyingi zaidi zinashiriki katika mashindano hayo, lakini kutokana na uhaba wa fedha zimeshindwa kufanya hivyo.

“Tumezipa nafasi zaidi kutafuta fedha ili kushiriki, tutafunga mlango wa kuthibitisha wiki moja kabla ya mashindano,” alisema Kapadia.

 Alisema kuwa Tanzania itashirikisha waogeleaji 60 wakigawanywa kwa timu mbili (Tanzania A na B) chini ya makocha wao, Alex Mwaipasi na Michael Livingstone.

Nchi ambazo zimeongezewa muda wa kuthibitisha kushiriki katika mashindano ni Ethiopia, Eritrea, Somalia, Rwanda, Sudani Kusini ambazi zipo kanda ya tatu na za kanda ya nne ni Angola, Botswana, Comoro, Madagascar, Lesotho, Malawi, Mauritius, Seychelles, Msumbiji, Namibia, Zimbabwe na Swaziland.

Alisema kuwa kwa kamati yao inatafuta wadhamini kwa ajili ya kufanikisha mashindano hayo. Wanahitaji kiasi cha Sh 100 milioni ili kufanya mashindano hayo kwa hadhi inayostahili.

Alisema kuwa wanatarajia waogeleaji zaidi ya 200 kushiriki katika mashindano hayo ambayo Tanzania ni mabingwa watetezi.

Mbali ya Kapadia, kamati hiyo pia unaundwa na wajumbe ambao ni Inviolata Itatiro, Geeta Gokarn, Phillip Saliboko, Imani Dominic, Hetal, Linges Ramasamy, Thauriya Diria, Amina Karume, Nitesh Patel, Nelly Coehlo na Mary Mugurusi.

0 comments: